Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkurugenzi wa UNESCO akasirishwa na shambulizi la kigaidi dhidi ya makavazi ya Mosul

Mkurugenzi wa UNESCO akasirishwa na shambulizi la kigaidi dhidi ya makavazi ya Mosul

Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO Bi Irina Bokova  amesema ameshtushwa na video iliyotolewa leo na kuonyesha uharibifu wa sanamu na kazi za Sanaa nyingine kwenye makumbusho ya Mosul.

Amesema analaani vikali shambulio hilo la makusudi dhidi ya historia na utamaduni huo wa kale wa Iraq kama ni kichocheo cha ghasia na chuki.

Ameongeza kuwa shambulio hilo ni zaidi ya janga la kitamaduni pia ni suala la kiusalama linalochagiza ubaguzi , ghasia za itikadi kali na mzozo nchini Iraq.

Bi Bokova amesema hatua hiyo inakiuka kabisa azimio la karibuni la baraza la usalama namba 2199 linalolaani uharibifu wa aina yoyote ile wa urithi wa kitamadini na usafirishaji haramu wa bidhaa za kale na vitu vya kitamaduni kutoka Iraq na Syria.

Amesema ndio maana amemjulisha mara moja Rais wa baraza la usalama kuitisha kikao cha dharura kuhusu ulinzi wa urithi wa kitamaduni wa Iraq kama kigezo kimojawapo cha usalama wa nchi.