Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asisitiza usitishwaji wa mapigano Syria

Ban asisitiza usitishwaji wa mapigano Syria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-moon amezitaka pande kinzani nchini Syria kusitisha mapigano  ili kuwapa ahueni raia wa nchi hiyo ambao wameteseka kwa muda mrefu.

Taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu inasema usitishwaji wa mapigano hima unahitajika kuelekea suluhisho la kisiasa la mgogoro huo. Ban anatoa wito huo kufuatia mwakilishi wake maalum nchini Syria Staffan de Mistura kuliambia baraza la usalama mnamo Februari 17 kuwa serikali ya nchi hiyo imeahidi kusitisha mashambulizi ya anga na makombora mjini Allepo kwa kipindi cha miezi sita ili kuruhudu Umoja wa Mataifa kufikisha misaada kuanzia mjini humo.

Amesema azimio la baraza la usalama namba  2139 lilitaka ukomeshwaji wa usambazwaji ovyo wa silaha katika makazi ya watu pamoja na urushaji wa makombora ya anga na hivyo kusema anatarajia serikali ya  Syria kutekeleza pia katika ahadi yake. Pia ametaka vikosi vya upinzani kutekeleza usitishwaji wa urushaji makombora mjini Allepo.

 Mgogoro wa Syria umesababisha vifo vya zaidi ya watu 200,000 pamoja na wakimbizi waliovunja rikodi ya idadi na pia kuzalisha vikundi vyenye misisamo mikali na vya kigaidi mathlani ISIL.