Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MINUSMA yachunguza vifo vilivyotokea Gao

MINUSMA yachunguza vifo vilivyotokea Gao

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA, unaanza kuchunguza vifo vilivyotokea wakati wa maandamano yaliyofanyika jumanne, mjini Gao.

Stephane Dujarric, msemaji wa Umoja wa Mataifa, amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mjini New York.

Amenukuu MINUSMA ikieleza kuwa ilitumia mabomu ya kutoa machozi na kufyatua risasi hewani ili kuzuia waandamanaji wasiingie kwenye jengo lake.

Wakati huo huo msemaji wa MINUSMA, Olivier Salgado, akizungumza na Redio ya Umoja wa Mataifa amesema hadi sasa watu wanne wamefariki dunia ilhali 13 wamejeruhiwa wakiwemo walinda amani wawili waliorushiwa mawe na waandamanaji.

(Sauti ya Olivier)

« Kitu muhimu cha kusema kwa sasa ni kwamba uchunguzi wa MINUSMA pamoja na mamlaka za serikali za kitaifa unaendelea ili kuhakikisha idadi ya wahanga na kujua ni vipi na pia na nani wamepigwa »

Maandamano hayo yalifanyika kupinga mpango wa MINUSMA wa kutekeleza makubaliano ya sitisho la mapigano na vikundi vilivyojihami vya Azawad kwa madai kuwa yalilenga kujisalimisha kwa waasi.

Hata hivyo MINUSMA inasema lengo la mpango huo ni kurejesha usalama kwenye maeneo ya Tabankort pekee na tayari imetangaza kusitisha utekelezaji wake.