Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban amkumbuka mfalme Abdullah wa Saudia kufuatia kifo chake

Ban amkumbuka mfalme Abdullah wa Saudia kufuatia kifo chake

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameelezea kuhuzunishwa na habari za kufariki dunia kwa Mfalme Abdullah Bin Abdulaziz Al-Saud wa Saudi Arabia hapo jana. Katibu Mkuu ametuma rambi rambi zake kwa familia ya Mfalme Abdullah, serikali na watu wa Saudia kufuatia kifo hicho.

Ban amesema Mfalme Abdullah alichangia pakubwa katika kuendeleza ufalme wa Saudia, akiongeza kuwa chini ya uongozi wake wa miongo mingi katika nyadhfa tofauti serikalini, ufalme huo umepiga hatua kubwa mno, na kuwaletea utajiri watu wake.

Ban amepongeza juhudi za Mfalme Abdullah katika kukabiliana na changamoto nyingi za kikanda na kimataifa wakati wa misukosuko na mabadiliko ya kasi, pamoja na katika kuendeleza mazungumzo baina ya dini tofauti duniani na mchakato wa amani wa mataifa ya Kiarabu.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson ameelekea nchini Saudi Arabia kuwakilisha Umoja wa Mataifa katika kutoa heshima kwa niaba ya Umoja huo kufuatia msiba wa mfalme Abdullah.