Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka wa nne wa vita Syria, UM warejelea wito wake

Mwaka wa nne wa vita Syria, UM warejelea wito wake

Mjumbe maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Staffan de Mistura amesema anataka kuona suluhu ya kisiasa mwaka huu wakati huu ambapo vita vya Syria vinaingia mwka wa nne .

Akiongea na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, de Mistura ameeleza kuwa na matumaini ya kufikia makubaliano baada ya kuongea na wadau wa pande zote, akisisitiza hali ya dharura ya kibinadamu nchini humo:

(De Mistura)

“ Watu milioni 12 wanahitaji msaada, watu 220,000 wameuawa, magonjwa ya kupooza, surua na homa ya matumbo yamerudi Syria, watoto milioni 3 hawaendi shuleni, Syria imeenda miaka 40 nyuma kulingana na sehemu ilipofika. Itahitaji labda muda ule ule kurudi kwenye hali yake tusipofanya haraka. Tumeanza mwaka 2015 kwa kuona Syria kama mzozo wa kwanza wa kibinadamu tangu mwisho wa vita vikuu vya pili.”

De Mistura ameongeza kwamba machafuko ya Syria yanaathiri pia nchi jirani hadi nchi zingine akitolea mfano wa mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea mjini Paris.

Amerejea wito wake wa kusitisha mapigano mjini Aleppo, kama hatua ya kwanza katika utaratibu wa amani.