Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ziarani India, Ban Ki-moon apongeza viongozi kwa hatua za kutunza mazingira

Ziarani India, Ban Ki-moon apongeza viongozi kwa hatua za kutunza mazingira

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amezindua kiwanda cha umeme unaotumia nishati ya jua, kwenye jimbo la Gujarat, nchini India, akipongeza juhudi za India katika kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Ameeleza kufuraishwa na maamuzi yaliyochukuliwa na serikali ya India ili kuongeza viwanda vinavyotumia nishati rafiki kwa mazingira, na kuleta umeme katika kila nyumba ya nchi kupitia nishati ya jua.

Alipozungumza na viongozi na wafanyabiashara wa India, Ban amesema dunia inahitaji kila nchi ichukue hatua ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuleta maendeleo endelevu yaliyokuwa marafiki kwa mazingira.

Aidha Ban Ki-moon ametembelea Ashram ya Sabarmati, ambayo ni nyumba ya makumbusho ya mkombozi wa India, Gandhi. Katibu mkuu amesema urithi wa Gandhi unapaswa kukumbushwa wakati dunia inakumbwa na ubaguzi, ugaidi na misimamo mikali, akimnukuu Gandhi aliposema : “ hapatakuwa amani ya kudumu duniani iwapo tutajifunza kuvumiliana na hasa kuheshimu dini ya watu wengine kama yetu”.