Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio dhidi ya AMISOM lalaaniwa vikali

Picha UN-AU / Stuart Price

Shambulio dhidi ya AMISOM lalaaniwa vikali

Baraza la usalama limelaani vikali shambulizi dhidi ya  kambi ya ujumbe wa Muungano wa Afrika nchini Somalia, AMISOM, ilioko katika kambi ya Halane, mjini Mogadiscio, hapo jana na kusababisha vifo kadhaa wakiwamo vya askari watatu wa AMISOM na raia mmoja mkandarasi.

Wajumbe wa baraza hilo wametuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga, kwa AMISOM na serikali ya Somalia.

Wamelaani vitendo vyote vinavyotekelezwa na Al Shabaab dhidi ya vituo vya AMISOM ambavyo vinafanya kazi na serikali na jeshi la Somalia katika kuwalinda raia na kusaidia katika ujenzi na utulivu wa nchi.

Wajumbe wa Baraza la usalama wamesisitiza nia yao ya kupambana na aina zote za ugaidi kwa mujibu wa wajibu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Ban Ki- Moon amelaani vikali shambulio hilo na kupongeza AMISOM kwa namna walivyojihami haraka.

Bwana Ban amesema amefahamishwa kuwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wako salama na hivyo kueleza mshikamano kati Umoja huo na  AMISOM kwa ajili ya amani ya Somalia.