Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kitisho cha ebola Afrika Magharibi kimezua balaa la chakula - FAO

Soko la chakula la Monrovia wilaya ya West point, 20 Agosti 2014.Picha@FAO

Kitisho cha ebola Afrika Magharibi kimezua balaa la chakula - FAO

Shirika la Kimataifa la Chakula na Kilimo FAO limesema kuwa mlipuko wa ugonjwa wa ebola katika nchi za Afrika Magharibi umesababisha maeneo hayo kukumbwa na tatizo la chakula. Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

FAO imesema shughuli za uzalishaji chakuka zimetatizwa na hivyo kusababisha chakula kilichopo kuuzwa kwa bei ya juu hali inayoweka katika hali ngumu wakazi wa maeneo hayo.

Mathalani ripoti zinaonyesha kuwa kuwepo kwa marufuku ya watu kusafiri ovyo katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone kumezorotesha shughuli zinazohusika na huduma za chakula.

Pamoja na kwamba marufuku hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti kusambaa kwa virusi vya ugonjwa huo lakini kwa upande wa pili umeathiri hali ya upatikanaji wa chakula.

Baadhi ya maeneo yameshuhudia watu wakinunua kwa wingi chakula hicho hatua ambayo imesababisha kupanda kwa haraka bei ya vyakula hivyo.

Hali ni mbaya zaidi katika maeneo ya mijini ambako ndiko kwenye mwingiliano mkubwa wa watu.

Wakati huo huo msimu wa mavuno ya mazao muhimu mpunga na mahindi unatazamiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa.

Msimu huo unaanza huku kukiwa na uhaba wa wafanyakazi jambo ambalo linaweza kusababisha kujitokeza kwa tatizo la ukosefu wa chakula hapo baadaye. Jonathan Pound ni afisa wa FAO anayehusika na tahadhari za mapema kuhusu  uhaba wa chakula.

(Sauti ya Jonathan)

“Wafanya biashara wengi wanahofia maambukizi , na hawataki kwenda maeneo ambayo kuna ugonjwa wa Ebola, na kwa sababu hiyo,  hawana uwezo wa kuleta bidhaa zao kwenye masoko makuu mijini, na wakulima hawawezi kuleta bidhaa zao katika masoko mengine madogo, hivyo hii ina athari kubwa ya mzunguko mzima wa usambazaji bidhaa kuanzia mashambani hadi masoko madogo na mwishowe masoko makubwa.”