Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM na AU zaazimia kuimarisha ushirikiano wao kwa amani Maziwa Makuu

UN

UM na AU zaazimia kuimarisha ushirikiano wao kwa amani Maziwa Makuu

Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wao katika kutekeleza mpango wa amani, usalama na ushirikiano kwenye maziwa makuu.

Hayo yamefikiwa huko Addis Ababa, Ethiopia baada ya mazungumzo kati ya Mjumbe maalum mteule wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye ukanda wa Maziwa Makuu Said Djinnit na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Muungano wa Afrika NkosazanaDlamini-Zuma.

Wawili hao wamekubailiana kuimarisha ushirikiano wa vyombo hivyo viwili katika utekelezaji wa mpango wa amani, usalama na ushirikiano wa Ukanda wa Maziwa makuu uliotiwa saini mwezi Februari mwaka jana huko Addis Ababa Ethiopia.

Bwana Djinnit pia amekuwa na mazungumzo na Kamishna wa amani na Usalama wa Muungano wa Afrika Smail Chergui na mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye muungano huo Haile Menkerios.

Wamejadili kuhusu uratibu na ushirikiano baina ya vyombo mbali mbali vya Umoja wa Mataifa katika kusaidia amani na maendeleo barani Afrika.

Ziara ya Djinnit ni sehemu ya kujitambulisha kwa viongozi wa Afrika na Ukanda wa Maziwa Makuu kufuatia kuteuliwa kwake karibuni kuchukua nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Mary Robinson ambaye amepatiwa jukumu lingine