Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICRC ndiyo inashughulikia msafara uliokwama huko mpakani Ukraine: Amos

Valerie Amos (Picha ya UM)

ICRC ndiyo inashughulikia msafara uliokwama huko mpakani Ukraine: Amos

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Bi. Valerie Amos yuko ziarani nchini Ukraine kujionea hali halisi ya kibinadamu kwenye mzozo unaoendelea na ambao hadi sasa unakadiriwa kusababisha watu 190,000 kupoteza makazi yao. Amina Hassan na taarifa kamili.

(Taarifa ya Amina)

Akizungumza katika mahojiano na Radio ya Umoja wa Mataifa, Bi. Amos amesema tayari amekuwa na mazungumzo na viongozi waandamizi akiwemo Waziri Mkuu na Naibu wake akisema kwamba amewakumbusha wao na pande zote kwenye mzozo huo wa Ukraine kuwa hali ya kibinadamu si nzuri na wanaosumbuka ni wananchi wa kawaida wasio na hatia.

Alipoulizwa kuhusu msafara wa zaidi ya malori 260 kutoka Urusi yaliyobeba shehena za misaada lakini yamezuiwa mpakani mwa Ukraine, Bi. Amos amesema..

(Sauti ya Amos)

“Suala zima la msafara wa magari linashughulikiwa na Kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu, ICRC. Umoja wa Mataifa haijahusishwa na mazungumzo hayo. Unaweza kuwa umeona taarifa iliyotolewa leo na ICRC, ikisema kuwa malori hayo yalivuka mpaka bila kusindikizwa na ICRC kwa sababu jana usiku walikuwa na wasiwasi sana na hali ya usalama eneo hilo.”

Mkuu huyo wa OCHA amesema kesho anakwenda eneo la Donetsk kujioneaa hali halisi.