Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza : Shule nyingine ya UN yapigwa na makombora ya Israel

Shule ya Jabalia iliyopigwa na makombora awali wiki hii. Picha ya Shareef Sarhan UNRWA

Gaza : Shule nyingine ya UN yapigwa na makombora ya Israel

Wapalestina 10 wamefariki dunia leo jumapili tarehe 3, kutokana na mashambulizi dhidi ya shule ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina, UNRWA, maeneo ya Rafah.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amelaani vikali mauaji hayo akisema ni ukiukwaji wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu, inayolazimu pande mbili za mzozo kuheshimu raia wa Palestina, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na majengo yake.

Ban Ki Moon ameongeza kwamba majengo ya Umoja wa Mataifa yanapaswa kuwa sehemu za usalama si za mapigano. Jeshi la Israel liliarifiwa mara nyingi kuhusu majengo hayo,  amesema, na uchunguzi unahitajika juu ya mashambulizi hayo, watekelezaji wakipaswa kuwajibika.

Katibu Mkuu ameleza kusikitishwa sana na ongezeko la ghasia na mauaji ya mamia ya Wapalestina huko Gaza. Amesema, utulivu unaweza kurejea kupitia mazungumzo ya amani baina pande zote na sitisho la mapigano.

Hatimaye, alirudia wito wake kwa pande zote kwa kusitisha mapigano sasa hivi na kufuatia tena njia ya amani.