Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ataka uchunguzi wa kudunguliwa ndege ya MH17 usitatizwe

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.Picha@UM

Ban ataka uchunguzi wa kudunguliwa ndege ya MH17 usitatizwe

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameelezea kusikitika kwamba wapelelezi wa kimataifa waliopewa jukumu la kuchunguza kudunguliwa kwa ndege ya Malaysia, MH17 wanaendelea kukabiliwa na vikwazo vya kufikia eneo la tukio hilo na kufanya kazi yao kwa sababu ya mapigano makubwa yanayoendelea katika eneo hilo.

Taarifa ya msemaji wake imesema kuwa bado kuna mabaki ya miili ya wahanga ambayo hayajapatikana, na kwamba kuna vitu vya ushahidi ambavyo bado vipo katika eneo hilo. Ban amesema familia za wahanga wanahitaji kutimiziwa matakwa yao, na ulimwengu unapaswa kuelezwa ni nini kilichotokea na kwa hiyo wachunguzi hao ni lazima waruhusiwe kutekeleza majukumu yao.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa pande husika kusitisha mara moja uhasama kwenye eneo la tukio, kulingana na azimio namba 2166 la Baraza la Usalama, ili kuwezesha timu za kimataifa kulifikia eneo hilo bila vikwazo vyovyote.