Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watu 1000 wameuawa Iraq: Ofisi ya Haki za Binadamu

Zaidi ya watu 1000 wameuawa Iraq: Ofisi ya Haki za Binadamu

Zaidi ya watu 1,000 wameuawa na wengine zaidi ya 1,100 kujeruhiwa nchini Iraq tangu Juni mwaka huu. Kwa mujibu wa Ofisi ya Haki za Binadamu na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, raia wapatao 757 waliuawa katika mikoa ya Nineveh, Diyala na Salahuddin kati ya tarehe 5 na 22 Juni. Taarifa kamili na John Ronoh

Taarifa ya John Ronoh

Ofisi ya Haki za Binadamu imesema bado kuna ripoti za utekaji nyara katika mikoa ya kaskazini na Baghdad, zikiwemo za utekaji wa raia wa kigeni. Baadhi ya watu waliotekwa wamepatikana wakiwa wameuawa, na inaaminika kuwa mauaji kinyume na sheria yanaendelea kutekelezwa. Rupert Colville ni msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu

“Idadi hii ambayo inapaswa kuchukuliwa kama ya chini zaidi, inajumuisha baadhi ya visa vya mauaji kinyume na sheria ya raia, polisi na wanajeshi waliokamatwa. Watu wengine 318 waliuawa na wengine 590 kujeruhiwa katika kipindi kicho hicho mjini Baghdad na maeneo ya kusini.”

Kundi lijulikanalo kama ISIS limetangaza video kadhaa zinazoonyesha unyama unaotendewa wanajeshi na polisi ambao wamekamatwa, ukiwemo kuwapiga risasi na kuwachinja, na watu wengine wanaolengwa kwa sababu za kikabila au kidini.

Wakati huo huo, Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF, limesema linaongeza juhudi za kuwafikishia watoto waliohama makwao usaidizi wa kibinadamu.