Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukame waweka maisha ya watoto milioni 4 hatarini Syria

Ukame waweka maisha ya watoto milioni 4 hatarini Syria

Maeneo ya Syria yanakumbwa na ukame, yakipokea mvua ndogo zaidi katika kipindi cha zaidi ya nusu ya karne, na hivyo kuyaweka maisha ya watoto zaidi ya milioni 4 hatarini, limesema Shrika la Kuhudumia Watoto katika Umoja wa Mataifa, UNICEF. UNICEF imesema kuwa juhudi zake zilizolenga kuingilia kati katika kukabiliana na matatizo ya maji na huduma za kujisafi, hazijapata ufadhili wa kutosha, kwani kufikia sasa imepokea asilimia 20 tu ya jumla ya ufadhili unaohitajika kwa mwaka 2014.

Uhaba wa maji nchini Syria umekithiri sasa, na UNICEF imesema huenda hali hiyo ikawalazimu raia wengi zaidi kuhama makwao, na hivyo kuongeza idadi ya watu milioni 6.5 ambao tayari wamefurushwa makwao na mzozo.

Halikadhalika, nchini Lebanon na Jordan, hali tete inaibuka baina ya wakimbizi wa Syria na wenyeji kutokana na kushindania rasilmali haba, yakiwemo maji. Ukame ulioko sasa, pamoja na miaka mitatu ya mgogoro ambao umeiharibu miundo mbinu nchini Syria, umechangia kwa kiasi kikubwa huduma za maji, na hivyo kupelekea UNICEF kutoa tahadhari kuhusu hali ya maji, usafi na huduma za kujisafi.