Hatua kubwa imepigwa Ufilipino baada ya kimbunga Haiyan: OCHA

27 Februari 2014

Tacloban ya leo ina tofauti kubwa na ile niliyoshuhudia mwezi Novemba wakati wa ziara yangu ya pili mwezi Novemba mwaka jana, amesema Mkuu wa shirika la misaada ya kiutu kwenye Umoja wa Mataifa, OCHA,  Valerie Amos alipozungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa ziara yake nchini humo Alhamisi. Ripoti ya Flora Nducha inafafanua zaidi.

 (Ripoti ya Flora)

Baada ya siku mbili nchini Ufilipino akipata fursa ya kukagua hali halisi kwenye maeneo yaliyopigwa zaidi na kimbunga Haiyan miezi minne ilopita, Bi.Amos amesema kuna matumaini, vifusi vya taka sasa vimepungua kwa kiasi kikubwa na kwingineko kazi ya kuondoa inaendelea, huduma za mawasiliano ikiwemo barabara zimerejea na hata biashara ndogondogo zimeanza na hivyo kuweka matumaini ya watu kujipatia kipato.

Amesifu mipango ya Ufilipino ya kupunguza madhara ya majanga ya asili akisema hatua hizo zimesaidia lakini bado kazi kubwa inahitajika.

 (Sauti ya Amos)

"Miezi tisa ijayo Umoja wa Mataiaf na wadau wetu wa kibinadamu hapa tunaweka vipaumbele vya makazi na mipango ya kujipatia kipato huku tukiendelea kuwapatia misaada ya kuokoa maisha na ulinzi kwa wale walio hatarini zaidi.Kuhamisha watu kutoka mahemani na makazi mengine baada ya vimbunga viwili kupiga tena maeneo yaliyokuwa yameathirika kumedhihirisha udharura wa kupatia suluhisho la kudumu la malazi kwa familia husika. Mahitaji ya shughuli za kujipatia kipato nayo ni makubwa mamilioni ya wakulima waliathiriwa na karibu theluthi mbili za jamii za wavuvi zilipoteza mali zao.”

Bi. Amos amesema serikali, Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia yanapaswa kuendelea kushirikiana zaidi ili watu walio hatarini zaidi waweze kujikwamua kimaisha wakati huu ambapo amesema wahisani wamejitoa kwa dhati kusaidia kwani ombi la dola Milioni 788 za usaidizi Ufilipino hadi sasa limechangiwa kwa asilimia 46.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter