Mwakilishi wa UM alaani shambulizi la bomu Beirut

27 Disemba 2013

Mratibu Maalum wa shughuli za Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, Derek Plumbly, amelaani vikali shambulio la bomu ambalo limemuua waziri wa wa zamani, Mohammad Chattah na watu wengine wapatao watano.

Katika taarifa ilotolewa leo, Bwana Plumbly ameelezea kushangazwa na kuhuzunishwa na shambulio hilo, huku akielezea sifa za Bwana Mohammad Chattah kama mtu mwenye busara, jasiri na mzalendo ambaye wakati wote alipendelea kuendeleza mashauriano na maslahi ya nchi nzima ya Lebanon.

Amepeleka risala za rambi rambi kwa jamaa na marafiki wa Bwana Chattah, na wa wahanga wote wa shambulio hilo la bomu.

Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha wale waliotekeleza kitendo hicho na vitendo vingine kama hivyo vya kigaidi wanakabiliwa kisheria, na haja ya utulivu wakati huu, huku akiwaomba raia wote wa Lebanon waungane kuunga mkono vyombo vya usalama vinapojaribu kuilinda nchi yao.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter