Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMID kuwezesha majadiliano baina ya Misseriya na Salamat Darfur:

UNAMID kuwezesha majadiliano baina ya Misseriya na Salamat Darfur:

Kufuatia mapigano baina ya Salamat na Misseriya katikati mwa Darfur yaliyokatili maisha ya watu zaidi ya 10 juma lililopita , mpango wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika wa kulinda amani Darfur (UNAMID) iliwezesha kusafiri kwa Wali gavana wa Darfur Kati na kamati ya taifa ya usalama. Watu hao wanaambatana na timu ya maafisa wa UNAMID kuelekea  Um Dukhun Jumapili Novemba 17 kwenda kupatanisha makabila hayo mawili.

Ujumbe huo ulikutana na kamati ya usalama ya eneo hilo, kamati ya amani na upatanishi pamoja na wawakilishi wa makabila ya Salamat na Misseriya katika juhudi za kusuluhisha mvutano uliopo na kuzitaka pande hizo mbili kuzingatia makubaliano ya amani yaliyotiwa saini 3 Julai 2013, kwa udhamini wa UNAMID.

UNAMID bado ina wasiwasi kuhusu athari za machafuko hayo ya kikabila kwa raia na itaendelea na juhudi za kushawishi pande hizo mbili kusitisha mapigano na kukumbatia amani ya muda mrefu.