IAEA na Iran zatangaza utaratibu wa ushirikiano

11 Novemba 2013

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki, IAEA, Yukiya Amano na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Iran, wametoa tangazo la pamoja la makubaliano ya utaratibu wa ushirikiano kuhusu suala la mpango nyuklia nchini Iran.

Tangazo hilo limesema IAEA na Iran zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wao na mazungumzo yenye lengo la kuhakikisha mpango wa nyuklia wa Iran ni wa amani pekee, kwa kutatua masuala yote yenye utata ambayo hayajatatuliwa na IAEA.

Kwa mantiki hiyo, Iran imekubali kuwa katika miezi mitatu ijayo, itashirikiana na IAEA katika shughuli za shirika hilo za kuhakiki na kutatua masuala yote ya sasa na ya zamani, ikiwemo kutoa taarifa kwa IAEA kuhusu mitambo yake ya nyuklia, na katika kutekeleza hatua za uwazi.

Kwa upande wake IAEA imekubali kuendelea kuzingatia hofu ya kiusalama ya Iran, ikiwemo udhibiti na utunzaji wa habari za siri.