IOM Uganda yafanikiwa kuwarejesha kwenye maeneo ya asili watoto waliorubuniwa

5 Novemba 2013

Shirika la Kimataifa la uhamiaji nchini Uganda IOM, likishirikiana na serikali ya Uganda, limefanikiwa kuwarejesha katika sehemu zao za asili watoto 21 ambao walikumbwa na biashara ya usafirishaji watu.

Idadi kubwa ya watoto hao wamekuwa wakisafirishwa kutoka eneo la Karamoja lililoko kaskazini mashariki mwa Uganda hadi mji mkuu wa Kampala na kutumikishwa kwenye shughuli za omba omba mitaani. Taarifa kamili na George Njogopa:

(TAARIFA YA GEORGE NJOGOPA)

Watoto hao kabla ya kurejeshwa kwenye maeneo yao ya asili walipatiwa msaada wa huduma mbalimbali ikiwemo matibabu, kulishwa chakula, na huduma nyingine muhimu.

IOM kwa kushirikiana na taasisi za kiraia ilichukua hatua za makusudi kwa kuandaa mazingira mujarabu huko Karamoja yaliyosaidia familia kuwatambua wanao ambao walikuwa tayari wamekubali kurejea nyumbani.

Pia kulilfanyika mafunzo maalumu ya kuzijengea uwezo familia hizo ili kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji.

Hata hivyo kuanzia sasa watoto hao watapitia mafunzo ya wiki tatu na baadaye wataunganishwa kwenye familia zao.

Tangu kuanzia mwezi Novemba mwaka 2011,shirika hilo la kimataifa limefanikuwa kuwarejesha katika hali zao za kawaida zaidi ya watoto 179 wa Karamoja ambao wamekuwa wakichukuliwa kwa ujanja ujanja na kupelekwa Mjini Kampala kutumika katika shughuli za uchuuzi.