Idadi ya watu wanaohitaji misaada nchini Syria yapanda hadi milioni 9.3: OCHA

5 Novemba 2013

Idadi ya watu wanaohitaji misaada nchini Syria imeripotiwa kupanda hadi kufikia milioni 9.3 . Kulingana na takwimu mpya kati yao hao watu milioni 6.5 wamekosa makazi lakini bado wako nchini humo.

Taarifa kamili na Grace Kaneiya

(TAARIFA YA GRACE KANEIYA)

Kiwango hicho ni tofauti na makadirio yaliyowekwa mwezi wa Juni, ambayo yalionyesha kuwa kingekuwa watu milioni 6.8 ili wale waliokosa makazi kingekuwa watu milioni 4.25. Ongezeko hilo lilitabiriwa na mapema kwani shirika la kimataifa linalohusika na uhamiaji lilionya hapo kabla kwamba iwapo mzozo huo unaendelea utakosa ufumbuzi hali ya ustawi wa kibinadamu inaweza kuwa mbaya zaidi nchini Syria.

Katika hatua nyingine, Mratibu wa mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kutoa misaada kwenye maeneo yanayokumbwa na majanga Valerie Amos, ameendelea kulitolea mwito baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutumia ushawishi wake kuzibana pande zinazohusika na machafuko hayo kutoa ulinzi kwa raia na mali zao.

Hata hivyo pamoja na upinzani unaoendelea kujitokeza, bado mashirika ya Umoja w Mataifa ya utoaji misaada yamefaulu kwa kiasi kusambaza misaada katika baadhi ya maeneo.

(SAUTI YA JENS LAERKE)

Idadi hiyo ya milioni 9.3 haijumuishi wakimbizi walioko nje. Ni wale wenye mahitaji ndani mwa nchi. Katika miezi kumi ya kwanza ya mwaka huu, kumekuwepo misafara ya misaada  34 ikiongozwa na Umoja wa Mataifa, ambayo imefika ama ngome za upinzani au maeneo yanayozozaniwa. Hivi sasa kuna mashirika na idara 15 za Umoja wa Mataifa zinazotoa huduma za kibinadamu nchini Syria."