Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS na usaidizi wa wafungwa wenye matatizo ya akili

UNMISS na usaidizi wa wafungwa wenye matatizo ya akili

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS unashirikiana na ofisi ya huduma kwa wafungwa nchini humo kusaidia wafungwa wenye matatizo ya akili.

Taarifa ya UNMISS imesema kwa sasa kuna wafungwa 118 wanaokabiliwa na tatizo hilo wengi wao wakiwa Juba, ambapo kati yao 104 ni wanaume na 14 ni wanawake.

Kwa mujibu wa mpango huo wa usaidizi, UNMISS inatekeleza mradi wa majaribio wa kuboresha afya ya akili ambapo hadi sasa wafungwa 60 wamepatiwa tiba kabla ya kuachiwa huru ilihali wengine wanaendelea kupatiwa matibabu.

Nchini Sudan Kusini wafungwa wenye matatizo ya afya ya akili wanajumuisha waliokamatwa kwa uhalifu wa kitabia, wanaokamatwa baada ya kuripotiwa na familia zao kutokana na tabia zao na wale wanaopata tatizo hilo wakiwa wanatumikia adhabu zao gerezani.