Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya mzozo Syria, UNICEF yahakikisha watoto wanasoma

Licha ya mzozo Syria, UNICEF yahakikisha watoto wanasoma

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, kwa ushirikiano na wizara ya elimu na wadau wengine nchini Syria, linaunga mkono kampeni ya kuhakikisha watoto wanarejea masomoni. Kampeni hiyo inalenga watoto Milioni Moja wa shule za msingi walioathiriwa na mzozo nchini mwao. Alice Kariuki na taarifa kamili.

(TAARIFA YA ALICE)

Huku mwaka mpya wa masomo ukianza nchini Syria watoto wengi wanakabiliwa na changamoto za kurudi shuleni. Ukiwa ni mwaka wake wa tatu mzozo ulio nchini Syria umeziacha karibu shule 4000 zikiwa zimeharibiwa au zikiwa makao kwa wakimbizi wa ndani. Kulingana na UNICEF kampeni hiyo inalenga kuongeza idadi ya watoto watakaojiunga na masomo ambao hawajapata masomo kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

UNICEF inasambaza mabegi na vifaa vingine vya masomo kama kalami na vitabu vya kuandika kwenye majimbo yote 14 nchini Syria. Wakati huo huo UNICEF inatoa vifaa vya masomo 5000 , 3000 vya kuchezea na 800 kwa watoto wanaoanza masomo. Ufadhili zaidi kwa sasa unahitajika ili kuwazesha watoto zaidi kuendelea na masomo nchini Syria na ni dola milioni 16 ambazo zimetolewa hadi sasa kati ya dola milioni 33 zilizoombwa.