UNICEF yahaha kuhakikisha watoto Syria wanasoma, licha ya machafuko.

3 Septemba 2013

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF linahaha kuhakikisha watoto walioathiriwa na machafuko nchini Syria wanapata elimu bila kujali ikiwa machafuko yataendelea katika siku za usoni au la.

Akiongea mjini Geneva msemaji wa UNICEF Marxie Mercado amesema watoto milioni 1.9 waliokuwa darasa la kwanza hadi la tisa waliacha shule katika mwaka wa masomo wa 2012 huku shule 3,000 zikiwa zimeharibiwa na zaidi ya 930 zinatumiwa kama makazi kwa wakimbizi nchini humo.

Katika kuhakikisha watoto wanakwenda shule katika hali hii ya sintofahamu Bi Mercado anaeleza mikakati ya UNICEF.

(SAUTI MERXIE MERCADO)

Kwa kushirikiana na wizara ya elimu na UNRWA, UNICEF wiki hii itazindua program yenye usalama ya kusomea nyumbani itakayowezesha watoto zaidi ya elfu nne katika eneo hili la mgogoro kuendelea kufuata mtaala wa taifa. Hili ni muhimu sana kwa kuwa elimu imepata pigo kubwa kwa kipindi cha miaka miwili na nusu ya mgogoro.Kuhakikisha kwamba watoto wanaweza kuendelea kusoma, hata kama ni kwa saa chache kwa siku inawalinda na kuwaweka katika maisha ya kawaida katika hali hii

.