WFP yatoa vocha za chakula kwa wakimbizi wa ndani Kordofan Kaskazini

7 Agosti 2013

Wiki mbili baada ya watu wa Kordofan Kusini kukimbia machafuko kwenye vijiji vya Kordofan Kaskazini shirika la mpango wa chakula WFP limewapa vocha za chakula takribani wakimbizi wa ndani 33,000.WFP na jumuiya ya mwezi mwekundu ya Sudan wamegawa vocha hizo kwenye maeneo 35 katika vitongoji vitatu. Grace Kaneiya na maelezo zaidi. (TAARIFA YA GRACE KANEIYA)

Kulipozuka machafuko hayo mwezi Aprili mwaka huu katika eneo la Abu Karshola, lililoko Kusini mwa Kordofan , idadi kubwa ya watu walilazimika kuomba hifadhi katika maeneo ya jirani ikiwemo katika jimbo la Kaskazini mwa Kordofan.

Mamia hao wa raia walilazimika kutembea kwa miguu kwa umbali mrefu na baadaye kuomba hifadhi ya kikimbizi katika eneo la El Rahat na kupata hifadhi kwa mwenyeji wa eneo hilo aliyetambulika kwa jina la Ibrahim Bobo .

Akizungumzia tukio la kuwapokea raia hao,Bobo alisema kuwa kutokana na mazingira ya eneo hilo, alipoteza familia zaidi ya tano lakini sasa amelazimika kuchukua hatua madhubuti ikiwemo kuwahamishia kwenye maeneo salama ili asipoteza familia zaidi.

Takwimu iliyofanywa na WFP,imeonyesha kuwa zaidi ya watu 30,000 wanahitaji msaada wa chakula na asilimia 60 ya raia hao ni watoto.