Ban awapongeza manusura wa Hiroshima na Nagasaki kwa kusambaza ujumbe wa madhara ya mabomu ya atomiki

6 Agosti 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametuma salamu zake kwenye mkutano wa kimataifa dhidi ya mabomu ya atomiki huko Geneva, Uswisi na kupongeza manusura wa mashambulio ya mabomu ya atomiki huko Nagasaki na Hiroshim ambao amesema kwa miaka Sitini na Minane wamekuwa wakipaza sauti juu ya madhara ya mabomu hayo.Bwana Ban amesema manusura hao wajulikanao kwa kijapani kama Hibakusha pamoja na kuelezea madhara wanayopata, pia husimulia vile walivyonusurika mashambulio hao na kwamba ujasiri wao umemtia yeye binafsi moyo wa kuendeleza jitihada za kutokomeza matumizi ya silaha za nyuklia.

Katibu Mkuu amesema kwa sasa dunia inashuhudia ongezeko la vilio vya kutaka matumizi ya mabomu ya Atomiki na Hidrojeni  kupigwa marufuku kutokana na utambuzi wa madhara yake na hivyo basi ushiriki wa maafisa wa serikali, mashirika ya kiraia na makundi kadhaa kwenye mkutano huo unasaidia kuendeleza lengo na azma ya kutokomeza silaha za nyuklia.

Amesema kutokomeza silaha za nyuklia kunawezesha kuelekeza matumizi ya rasilimali adhimu kwenye matatizo makubwa yanayokumba dunia kama vile umaskini, njaa na magonjwa na hivyo basi kwa kufanya hivyo dunia itakuwa inachangia kufikiwa kwa malengo ya maendeleo ya milenia mwaka 2015 na kuwa na mustakhbali bora kwa wakazi wote wa dunia hii.