Mashambulizi dhidi ya walinda amani yanaweza kuwa ni uhalifu wa vita:ICC

19 Julai 2013

Mwendesha mashitaka kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC Fatou Bensouda amelaani mauaji ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania na kujeruhi wengine 17 wakiwemo wanajeshi na polisi wanaouunda kikosi cha pamoja cha Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika UNAMID.

Watu hao waliuawa tarehe 13 Julai huko Kusini mwa Darfur Sudan baada ya walinda amani hao waliokuwa kwenye doria kushambuliwa na watu wasio julikana.

Mwendesha mashitaka anakumbusha pande zote kwenye mgogoro wa Sudan kwamba ICC ina mamlaka na Darfur kwa mujibu wa azimio la baraza la usalama namba 1593, na kwamba kwa ajili hiyo basi mashambulizi ya makusudi dhidi ya walinda amani yanaweza kuchukuliwa kama uhalifu wa vita.

Ameongeza kuwa ofisi yake haitosita kuchunguza na kuwachukulia hatua wanaodaiwa kutekeleza uhalifu huo endapo uongozi wa serikali waliyoko umeshindwa kufanya hivyo.

Mwendesha mashitaka ameitaka serikali ya Sudan kufanya uchunguzi wa kina na wa haraka , na kuwafikisha kwenye mkono wa sheria wahusika wa shambulio hilo. Shambulio hilo linafanya idadi ya walinda amani wa UNAMID waliouawa tangu mwaka 2007 kufikia 54.