Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za kikanda zichukuliwe kuboresha usafi wa hewa maeneo ya Asia na Pasifiki: UNESCAP

Hatua za kikanda zichukuliwe kuboresha usafi wa hewa maeneo ya Asia na Pasifiki: UNESCAP

Mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Kiuchumi na Kijamii kwa ukanda wa Asia na pasifiki, ESCAP, Dr. Noeleen Heyzer, ametoa wito kwa nchi katika ukanda huo kutoa kipaumbele kwa usafi wa hewa na afya ya mwanadamu.

Dr. Heyzer amesema afya ni kichochezi muhimu cha maendeleo, na kuongeza kuwa, katika juhudi za kujenga ukanda endelevu, ni lazima kuhakikisha kuwa kuzuia uchafuzi wa hewa, maji, chakula na vitu vingine vinavyotumiwa na ukanda kwa ujumla ni vitu vya kipaumbele vya kiwango cha juu.

Mkuu huyo wa ESCAP amesema hakuna maana kuwekeza katika mifumo ya afya na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya na wakati huo huo, gharama ya ukuaji ni uharibifu wa rasilmali za kimsingi za mazingira ambazo ndizo tegemeo la afya ya mwanadamu. Amesema ni vyema kukumbuka kuwa mojawapo ya hatari kubwa kabisa zitokanazo na uchafuzi wa hewa, hususan katika miji inayoendelea kupanuka kwa kasi, ni chembechembe zinazoongeza hatari ya magonjwa ya moyo na mapafu, pamoja na saratani.