Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjumbe wa katibu mkuu wa UM ataka kusitishwa mapigano mjini Kismayo

Mjumbe wa katibu mkuu wa UM ataka kusitishwa mapigano mjini Kismayo

Mjumbe maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Nicholas Kay ametaka kusitishwa kwa mapigano mjini Kismayo kufutaia kuripotiwa tena kwa mapigano . Kay anazitaka pande zote husika kutatua tofauti zao kwa njia ya amani. Anasema kuwa hali ya sasa nchini Somalia inastahili kuwa ambayo matatizo yanatatuliwa kwa njia ya amani.

Anasema kuwa ghasia husababisha watu kuteseka zaidi na huchelewesha yale yanayofanywa na jamii ya kimataifa. Mjumbe huyo wa katibu mkuu anasema kuwa ujumbe wa Umoja wa Matifa nchini Somalia UNSOM umesema kuwa utachukua wajibu mkubwa katika kutatua mizozo ya kisiasa ya kila aina kupitia ushauri kwa pande husika. Kay alichukua wadhifa wake tarehe tatu mwezi huu kama mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia UNSOM.