Mzozo wa Israeli-Palestinian usipuuzwe kwa kutupia macho zaidi mapigano ya Syria:UM

23 Mei 2013

Afisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa ameonya jumuiya ya Mataifa kuendelea kutupia macho mzozo wa Syria huku ikikawia kutafutia ufumbuzi  mzozo wa muda mrefu baina ya Israel na Palestina.

Robert Serry ambaye ni mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Mashariki ya Kati ambayeliambia baraza la usalama kuwa hali jumla kwenye eneo hilo siyo ya kuridhisha.

Amesema kuwa ustawi wa eneo la Mashariki ya Kati unatumbukia kwenye kipindi kibaya na chakutisha ikiwemo kuvurugwa kwa hali za kibinadamu.

Mwanadiplomasia huyo amesema kuwa hali ya wasiwasi kwenye eneo hilo inaendelea kumea mizizi huku umwagaji wa damu ukiendelea kushuhudiwa nchini Syria. Ameongeza kuwa kumekuwa na ongezeko la mapigano ikiwemo pia katika eneo la Goran ambako vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kulinda amani vimepiga kambi.