Leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza Fistula

23 Mei 2013

Kwa mara ya kwanza dunia hii leo inaadhimisha siku ya kutokomeza fistula, hali ambayo inampata mwanamke aliyekaa na uchungu muda mrefu kabla ya kujifungua kutokana na kukosa huduma za uzazi haraka au mtoto wa kike ambaye bado hajakomaa kuweza kujifungua. Hali hii husababisha mzazi kuchanika sehemu za siri na hivyo kutokwa na haja ndogo na haja kubwa mfululizo.Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la idadi ya watu la Umoja wa Mataifa Dkt. Babatunde Osotimehin amesema ni masikitiko makubwa kuwa wanawake na watoto wa kike maskini wako hatarini zaidi kupata fistula, na mara nyingi ni vigumu kuweza kuwapatia tiba. Amesema ugumu huo unatokana na unyanyapaa dhidi yao na wengi wao hawana taarifa juu ya uwezekano wa kutibiwa fistula wakati katika nchi tajiri hali hiyo inazuilika na hata kama mzazi akipata baada ya kujifungua anaweza kufanyiwa upasuaji na kupona.

Dokta Robert Marenga ni mtaalamu wa kutibu Fistula katika hospitali ya CCBRT nchini Tanzania na hapa anaeleza hali ilivyo kwa Tanzania.

(SAUTI Dokta Marenga)

Mwaka jana, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitenga tarehe 23 mwezi Mei kuwa siku ya kimataifa ya kutokomeza fistula ambayo ni hali ya mwanamke kuchanika wakati wa kujifungua na kusababisha kushindwa kuzuia haja ndogo.