Baraza la Usalama lajadili hali ya usalama Jamhuri ya Afrika ya Kati

15 Mei 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limepokea ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu hali ya usalama huko Jamhuri ya Afrika ya Kati na mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa kufuatia kuzorota kwa usalama tangu waasi wapindue serikali. Joshua Mmali na taarifa zaidi.(Taarifa ya Joshua)

Akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, Margare Vogt, amesema taasisi za mpito zilizowekwa katika nchi hiyo kufuatia kupinduliwa kwa serikali, ni hafifu na zinahitaji msaada wa haraka kutoka jamii ya kimataifa.Akiongea kuhusu hali ya usalama, Bi Vogt amesema hali inaendelea kuzorota, na kuwa mbaya zaidi hususan katika mji mkuu wa Bangui, ambapo uporaji bado unaendelea, na shule nyingi na biashara bado zimefungwa.
 
Amesema hali mbovu ya usalama nchini humo inatishia usalama wa ukanda mzima, kwani hatari ya kusambaza kwa silaha imeongezeka, ikichukuliwa kuwa waasi wa Seleka wamesaidiwa na makundi yenye silaha kutoka nje ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.Bi Vogt pia amesema katika ripoti yake kuwa hali ya haki za binadamu imeendelea kuzorota tangu waasi wa Seleka walipotwaa mamlaka, huku mahitaji ya kibinadamu yakizidi kuongezeka.
 
(SAUTI YA BI. VOGT)
 
"Ukatili na ukiukwaji haki unaotekelezwa na vikosi vya Seleka na makundi mengine yalojihmai, ukiwemo ubakaji, mauaji na kulemaza pamoja na kuajiri watoto katika jeshi na kuwalazimu kuwaoa kwa lazima ni suala la kutia wasiwasi kuhusu ulinzi wa raia. Pia ni ukiukwaji mkubwa wa sheria ya kimataifa ya haki za binadamu nay a kibinadamu. Hali katika Jamhuri ya Kati ni mbovu, ya kutisha na isokubalika."

Bi Vogt amesema Jamii ya kimataifa inatakiwa  kupeleka ujumbe mkali kwa viongozi wa Seleka kwamba hawawezi kukwepa mkono wa sheria kwa mauaji, uporaji na kubadilisha serikali kinyume na katiba.