Uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu WTO wafikia ukingoni, mtarajiwa ataja vipaumbele

8 Mei 2013

Wakati Mkutano maalum wa Baraza Kuu la shirika la biashara duniani, WTO ukitarajiwa kuitishwa tarehe 14 mwezi huu kuteua rasmi Mkurugenzi mkuu mpya wa shirika hilo, mmoja wa wagombea ambaye amepigiwa chepuo la kuchukua wadhifa huo Roberto Azevedo ametaja mambo muhimu yanayopaswa kupatiwa kipaumbele.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Radio ya Umoja wa Mataifa, Azevedo kutoka Brazil ametaja kipaumbele kuwa ni kuondoa mkwamo wa mazungumzo ya biashara WTO.

(SAUTI YA ROBERTO)

“Nafikiri moja ya vipaumbele vya Mkurugenzi Mkuu vitakuwa ni kuondoa mkwamo wa mazungumzo, shirika lipo katika hali ya mdororo na kwa kiasi kikubwa ni kutokana na kwamba hatuwezi kusongesha mbele mazungumzo hadi kusababisha kila kitu kwenye shirika kimekwama vile vile. Ajenda yote ya biashara na majadiliano yote ya biasharaya kisasa ambayo yanapaswa kufanyika, hayafanyiki. Ili kuondoa mkwamo huo tunapaswa kuibuka na jibu kutoka mkutano wa mawaziri huko Bali mwishoni mwa mwaka."

Kinyang’anyiro cha nafasi ya Mkurugenzi Mkuu kilikuwa na wagombea tisa kutoka Brazili, Jamhuri ya Korea, Mexico, Jordan, Costa Rica, New Zeland, Ghana, Indonesia na Kenya.

Mkurugenzi Mkuu wa sasa Pascal Lamy atahitimisha kipindi chake tarehe 31 mwezi Agosti mwaka huu.