Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanajeshi Mali wapewa mafunzo

Wanajeshi Mali wapewa mafunzo

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa lile la wakimbizi, UNHCR , pamoja na ofisi ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA yameendesha mafunzo kwa askari na wanajeshi nchini Mali kuhusu haki za binadamu na sheria za kimataifa.

Mafunzo hayo yameandaliwa kuwawezesha maafisa wa jeshi kuelewa tofauti kati ya wapiganaji na raia, ulinzi dhidi ya wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu, watoto, wakimbizi, wakimbizi wa ndani na maafisa wa kiraia, marufuku ya kwachukua mateka,kutesa pamoja na kujihusisha katika uporaji na ufyatuaji wa risasi hovyo.

Mafunzo hayo ambayo yamehusisha wanajeshi 600 wa Mali katika eneo liitwalo Koulikoro,yamedhaminiwa na Umoja wa Ulaya ambapo mafunzo hayo yanatarajia kuwajumuisha wapiganaji 3000 watakaopelekwa Kaskazini mwa Mali kwa ajili ya kulinda amani.

Afisa wa ulinzi kutoka UNHCR Pierre Jacques ambaye aliendesha mafunzo amesema wanajeshi wameelewa sio tu umuhimu wa kulinda raia lakini pia kutenda haki kwa watu wote wa Mali.

Mgogoro unaoendelea Mali umesababisha wakimbizi zaidi ya laki moja na elfu sabini na tano ambao wako katika nchi mbalimbali zikiwemo Mauritania, Niger, Burkina Faso na Algeria hii ikiwa ni kwa wale waliojiandikisha pekee.