Afrika isaidiwe kutatua mizozo kwa njia ya amani: Umoja wa Mataifa

25 Aprili 2013

Juhudi za kutatua mizozo kwa njia ya amani,Afrika

Ulimwengu unatakiwa kujitolea, na kwa ari zaidi, ili kusaidia kumaliza migogoro ambayo imeendelea kuyakatili maisha ya watu wengi barani Afrika. Kauli hiyo imetolewa na rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Vuk Jeremic, wakati wa kikao maalum cha Baraza hilo kinachoangazia suala la utatuzi wa mizozo kwa njia ya amani barani Afrika. 

Bwana Jeremic amesema hali nchini Mali, mashariki mwa DRC, na Jamhuri ya Afrika ya Kati bado zinatia wasiwasi. Ameongeza kuwa ingawa kumekuwa na ufanisi mkubwa kutuliza hali Somalia, Sudan na Sudan Kusini, hali katika ukanda wa Sahel bado ni tete na inahitaji pia juhudi zaidi

Nikizingatia juhudi zinazofanywa kusuluhisha mizozo hii, sidhani kama jamii ya kimataifa inazingatia ipasavyo hali tatanishi ya usalama inayolikabili bara la Afrika- tokea ugaidi, matishio ya uhalifu wa kimataifa wa kupangwa, hadi uzagaaji wa silaha, ujenzi wa amani na uhamiaji wa halaiki.

Nina imani ya dhati kuwa tunatakiwa kusaidia masuluhu yanayobuniwa na Wa-Afrika kwa changamoto zote zinazoikabili Afrika.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameliambia Baraza hilo Kuu kwamba bara la Afrika limepiga hatua kubwa tangu nchi zake nyingi zipate uhuru, kwani hata sasa lina chumi saba kati ya kumi zainazokua kwa kasi zaidi kote duniani.

 Akisifu hatua zilizopigwa kutatua migogoro kwa njia ya amani katika nchi kadhaa, Bwana Ban amehimiza kuwepo mikakati jumuishi

Utatuzi wa mizozo Afrika au kwingineko duniani hauwezi kuwa tu wajibu watu wa tabaka la juu.

Jamii ni lazima zihisi zinahusishwa katika mikakati na harakati zote. Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa zinaweza na ni lazima zitafute masuluhu ya kudumu na kuimarisha uwezo wa wote kufanikisha masuluhu ya amani, hasa wanawake.