Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubinafsishaji sekta ya Kahawa Burundi usubiri kwanza: Mtaalamu

Ubinafsishaji sekta ya Kahawa Burundi usubiri kwanza: Mtaalamu

 

Wataalamu wawili wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya chakula na deni la nje wametaka kusitishwa kwa utekelezaji wa sera za ubinafsishaji wa sekta ya kahawa nchini Burundi zinazoongozwa na Benki ya dunia hadi pale tathmini ya madhara yake kwa haki za binadamu utakapofanyika. Grace Kaneiya na maelezo zaidi.(RIPOTI YA GRACE)

Mapato yatokanayo na zao la kahawa nchini Burundi ambayo ni ya tatu kwa umaskini duniani, yanatoa picha halisi ya pengo kati ya usalama wa chakula na tatizo la njaa ambalo linawaandama wananchi wengi.

Licha ya hali hiyo, serikali iko mbioni kufanyia marekebisho sekta ya kahawa kwa mujibu wa sera za Benki ya Dunia ambapo mtaalamu maalumu wa Umoja wa Mataifa juu ya haki ya chakula, Olivier De Schutte ameonya kuwa hatua hiyo inaweza kuvuruga ustawi wa kijamii.

Amegusia sera za awali za marekebisho ya kiuchumi za Benki hiyo za kati ya miaka 80 hadi 90 ambazo zililazimu serikali kuuza mali zake.

Amesema sera hizo hazikuwa na manufaa yoyote kwa mwananchi na hivyo hazipaswi kurejelewa tena kwani ziliwatia wananchi maskini kwenye mazingira magumu.

Ametolea mfano mwaka 2008hadi 2009 ambapo inadaiwa chini ya shinikizo la benki ya dunia, sekta ya kahawa ilibinafsishwa na wakulima wa kawaida kujikuta wanashindwa kuboresha kilimo chao kutokana na kupanda kwa gharama.