Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban awasihi Wakenya kukamilisha kura kwa amani

Ban awasihi Wakenya kukamilisha kura kwa amani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametoa wito kwa watu wa Kenya kulinda amani na kutoa nafasi ya kumalizika kwa shughuli ya uchaguzi nchini humo kwa njia ya kuaminika, wakati huu wanaposubiri kumalizika kuhesabiwa kwa kura, kinyume na mambo yalivyokuwa mwaka 2007.

Bwana Ban amewaambia waandishi wa habari mjini Neww York kwamba ametiwa moyo na kuendeshwa kwa shughuli ya uchaguzi kwa njia ya amani na taratibu, licha ya matukio machache ya ghasia na matatizo ya kiteknolojia.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa wale walopiga kura, pamoja na wanasiasa walochuana kwenye kura hiyo na wafuasi wao kuwa watulivu na wenye subira, ili wairuhusu tume ya uchaguzi kukamilisha kazi yake ya kuhesabu kura.

“Jizuie kutokana na matamshi yoyote ambayo yanaweza kuiondolea heshima tume hiyo au kusababisha utata. Kukamilisha uchaguzi kwa amani na uaminifu vi mikononi mwa Kenya, na itakuwa hatua muhimu kwa demokrasia na maendeleo yake”

Mamilioni ya Wakenya walijitokeza kupiga kura mnamo Jumatatu wiki hii, ukiwa ndio uchaguzi wa kwanza tangu ule wa mwaka wa 2007 uliofuatiwa na machafuko na mauaji ya zaidi ya watu elfu moja, pamoja na kuwalazimu wengine zaidi ya laki sita kuhama makwao.