Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban azindua ziara rasmi za watoto ndani ya Makao Makuu ya UM

Ban azindua ziara rasmi za watoto ndani ya Makao Makuu ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amezindua rasmi ziara za watoto ndani ya Umoja huo mjini New York Marekani na kusema kuwa ziara za namna hiyo ni fursa ya kuelezea watoto jinsi Umoja wa Mataifa unavyofanya kazi kuboresha maisha ya wakazi mbali mbali duniani na wao wataeneza taarifa hizo.

Amewaeleza watoto hao kuwa Umoja wa Mataifa wenye nchi wanachama 193 unaweza kusaidia watoto kusoma hata kwenye mazingira yasiyo na madarasa, kusaidia wanawake na watoto wa kike walio kwenye mateso na hata kulinda na kujenga amani kwenye nchi zenye migogoro.

Hata hivyo amesema watoto ambao ni madaktari, wanasiasa na hata waigizaji wa baadaye wanahitaji udadisi zaidi, hamasa na fikra pana kuweza kufahamu shughuli za Umoja wa Mataifa.

Ameeleza kuwa Umoja wa Mataifa siyo sehemu ya kukutanisha serikali bali chombo hicho kipo kwa ajili ya watu wote wakiwemo watoto, walimu wao na hata familia na hivyo amewasihi kuwaelezea watu wengine kile watakachoshuhudia wakati wa ziara hiyo.