Skip to main content

UM wataka haki itendeke Bangladesh kwa watuhumiwa wa uhalifu

UM wataka haki itendeke Bangladesh kwa watuhumiwa wa uhalifu

Wataalamu huru wawili wa Umoja wa Mataifa wameonyesha wasiwasi wao vile ambavyo Bangladesh inasikiliza na kuhukumu watuhumiwa wa vitendo vya zamani vya uhalifu na wametaka haki itendeke.

Wataalamu hao wa haki za binadamu Christof Heyns, na Gabriela Knaul wameonyesha wasiwasi wao kufuatia mwenendo wa mashauri yaliyotangulia ambapo watuhumiwa Abdul Kalam Azad alihukumiwa adhabu ya kifo bila kuwepo mahakamani na Abdul Kader Molla akihukumiwa kifungo cha maisha jela.

Wataalamu hao wamesema mwenendo wa kesi umetia mashaka na hata kutia hofu kuwa kesi nyingine ambazo bado hazijasikilizwa na mahakaam ya kimataifa ya uhalifu ya Bangladesh iliyoundwa na serikali mwaka 2010 unaweza kuhitimishwa na adhabu za aina hiyo.

Mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi dhidi ya watuhumiwa wa makosa ya mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu ikiwemo vitendo vilivyotokea wakati wa vita vya uhuru mwaka 1971.

Wamesema mahakama hiyo ni muhimu kushughulikia uhalifu lakini ni lazima ihakikishe watuhumiwa wanapata haki ikiwemo kuzungumza na mawakili wao na hata kuita mashahidi watakaozungumza kwa niaba yao.