Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aorodhesha mambo ya kipaumbele katika ajenda ya mwaka 2013

Ban aorodhesha mambo ya kipaumbele katika ajenda ya mwaka 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, leo ameliambia Baraza Kuu la Umoja huo kwamba, masuluhu ya kudumu kwa matatizo ya dunia hayawezi kamwe kuachwa katika mikono ya serikali pekee, na kwamba Umoja wa Mataifa katika karne ya 21 ni lazima uangazie mitandao na ushirikiano.

Bwana Ban amesema maamuzi yanayofanyika au kushindwa kufanyika katika miaka michache ijayo, yataathiri ulimwengu kwa miongo mingi baadaye. Amesema Baraza Kuu linakutana wakati ulimwengu ukiyumbayumba, kufuatia migogoro barani Afrika na Mashariki ya Kati, pamoja na mdororo wa kiuchumi na mazingira kote duniani.

Katibu Mkuu ametaja migogoro na matatizo yanazozikumba nchi za Syria, Mali, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, pamoja na amani Mashariki ya Kati kati ya Israel na Palestina kama mambo ya kipaumbele katika mwaka huu.

(SAUTI YA BAN KI-MOON)

Tunapewa mtihani kila siku. Matumaini yangu na mahitaji yetu ya pamoja ni kuona kuwa tunakomesha mwendo wa mzozo baada ya mzozo na badala yake kukabiliana na vianzo vya matatizo haya, na kutambua kasoro zilizopo katika mbinu zetu za utendaji kazi. Matatizo ya sasa, mashinikizo kwenye ardhi na uchungu wa watu wetu- vyote hivi vinatuhimiza kufanya vyema zaidi katika mwaka huu.