Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baridi kali ya dhoruba yataabisha wakimbizi wa Syria

Baridi kali ya dhoruba yataabisha wakimbizi wa Syria

Mabadiliko ya hali ya hewa yaliyokumba nchi za Lebanon, Jordan na  Iraq ambazo zimekubwa na mvua kubwa iliyoambatana na theluji kali, imetajwa kuvuruga ustawi wa wakimbizi wengi wa Syria.

Kumekuwa na uharibifu mkubwa katika kambi ya Za’atari iliyoko kaskazini mwa Jordan ambako mahema pamoja na mifumo ya upitishaji maji imevurugwa.

Mamia ya wakimbizi wengi wao wakiwa watoto wapo katika hali mbaya na tayari shirika la Umoja wa Mataifa la watoto UNICEF limeanzisha juhudi za kukwamua hali hiyo mbaya.

Kiasi cha wakimbizi 55,000 nusu yao ikiwa ni watoto wanaishi kwenye kambi hiyo iliyovurugwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Jordan  Dominique Hyde amesema kuwa juhudi za kuwakwamua wakimbizi hao zinakwazo kutokana na ukosefu wa fedha na ameitolea mwito jumuiya ya kimataifa kutoa misaada ya dharura.