Surua bado tishio baadhi ya maeneo licha ya mafanikio: WHO

Surua bado tishio baadhi ya maeneo licha ya mafanikio: WHO

Shirika la afya duniani, WHO limesema licha ya dadi ya vifo vitokanavyo na Surua kupungua kwa asilimia 71 kati ya mwaka 2000 na 2011 duniani, ugonjwa huo bado ni tishio baadhi ya maeneo.

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa Alhamisi na WHO ambapo kwa mwaka 2000 kulikuwa na vifo 542,000 ikilinganishwa na vifo 158,000 mwaka juzi.

Halikadhalika idadi ya wagonjwa wapya ilipungua katika kipindi hicho kutoka 853,000 hadi 355 000. Ukanda wa Amerika na Pasifiki Magharibi zimetajwa kuwa katika mwelekeo wa kutokomeza Surua ilhali milipuko mipya ya Surua ikikwamisha mafanikio katika maeneo.

Dkt. Robert Perry ni mtaalam kutoka WHO.

(SAUTI YA Dkt. Perry)

“Tunafahamu kuwa katika baadhi ya maeneo kuna kusita au kupuuza suala la watoto kupatiwa chanjo. Kwenye nchi nyingi kuna makundi ya watu ambayo hayahdumiwa vizuri na mfumo wa afya au na mfumo wa kawaida wa chanjo. Na vile vile kuna nchi nyingnie ambazo zina matatizo ya kuwapatia watu wake wote huduma za afya na hiyo ni kutokana na ukosefu uwa rasilimali unaosababishwa na ukosefu wa utulivu wa nchi.”

 WHO inapendekeza kila mtoto apate vipimo viwili vya chanjo dhidi ya Surua ambapo Dkt. Perry amesema India imeandaa mpango wa chanjo hiyo huku Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ikiongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wasio na chanjo dhidi ya Surua.