Mapigano yasababisha watu zaidi kukimbia Mali

15 Januari 2013

Makabiliano kati ya jeshi la Mali linaloungwa mkono na ufaransa dhidi ya wanamgambo wa Al-Qaida kwenye maeneo ya Konna, Lere na Gao kaskazini mwa Mali yamesabisha kuhama kwa watu ndani na kwenda nchi majirani zake.

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR linasema kuwa zaidi ya watu 648 kwa sasa ni wakimbizi wa ndani huku watu wengine 309 wakiwa wameingia nchini Burkina Faso huku wengine 471 wakiripotiwa kuwasili kwenye kituo cha Fassala karibu na mpaka wa Mali.

Adrian Edwards ni msemaji wa UNHCR.

“Wakimbizi wanatueleza kuwa wanakimbia mapigano yanayoendelea halikadhalika ukosefu wa fursa na huduma za msing, na kulazimishwa kutekeleza sheria ya kiislamu, Sharia. Asilimia Tisini ya waliokimbia na ambao wamewasili kwenye maeneo kama wakimbizi ni wanawake na watoto kutoka maeneo ya Lere huko Mali. UNHCR imetoa mpango mpya wa kushughulikia hali ya sasa iwapo wakimbizi zaidi watakimbilia nchi jirani na hata ndani ya Mali na tuko tayari kutoa msaada kadri inavyohitajika.”

Kulingana na Edwards UNHCR kwa sasa inakabiliwa na uhaba wa fedha ikiwa imepokea asilimia 63 kati ya dola milioni 123 ilizoomba za kuwasaidia wakimbizi wa ndani nchini mali mwaka uliopita.