Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asikitishwa na vifo vya watu 61 huko Cote D’Ivoire

Ban asikitishwa na vifo vya watu 61 huko Cote D’Ivoire

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- Moon ametuma salamu za rambi rambi kwa serikali  ya Cote D’Ivoire na familia, jamaa na ndugu wa watu 61 waliopoteza maisha kufuatia kuibuka kwa kizazaa na msongamano baada ya sherehe za mwaka mpya huko Abidjan, nchini humo.

Msemaji wa Ban amemkariri Katibu Mkuu huyo akisema kuwa amesikitishwa na vifo hivyo ambapo pia watu wapatao 50 walijeruhiwa wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Mapema Mwakilishi maalum wa Bwana Ban nchini Côte d’Ivoire Bert Koenders alikaririwa akisema kuwa mkasa ho umesababisha majonzi kwa raia wa nchi hiyo wakati wakisherehekea ujio wa mwaka mpya wa 2013 uliobeba matumaini makubwa ya ujenzi wa amani, maridhiano na kujikwamua kiuchumi na kisiasa kwa wananchi wote wa Cote D'Ivoire.

Amekaririwa akisema kuwa mara baada ya kupata taarifa za mkasa huo, ofisi hiyo ilituma jopo la wahudumu wa dharura pamoja na kutangaza utayari wa kusaidia wahanga na uchunguzi wa tukio hilo.