Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Eritrea ionyeshe ushirikiano kushughulikia haki za binadamu: UM

Eritrea ionyeshe ushirikiano kushughulikia haki za binadamu: UM

Mtaalamu mpya wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Eritrea Beedwantee Keetharuth ametaka nchi hiyo kuonyesha ushirikiano wa kushughulikia haki za binadamu nchini humo kwa mujibu wa Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa.

Taarifa ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imemkariri Bi. Keetharuth akisema ni matumaini yake kuwa serikali ya Eritrea itazingatia mamlaka yake kama mtaalamu mpya kama fursa ya kuanza tena mashauriano kuhusu masuala ya ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo yaliyoibuliwa na jumuiya ya kimataifa na wadau wengine.

Mtaalamu huyo aliyeteuliwa mwezi Septemba mwaka huu, anatarajiwa kuwasilisha ripoti yake mbele ya baraza la haki za binadamu la Umoja wa mataifa mwezi Juni mwakani na amesema tayari ameomba kufanya vikao na wanadiplomasia wa Eritrea walioko Uingereza na Uswisi. Mapema mwakani atakwenda Eritrea.