Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya wasyria nusu milioni sasa ni wakimbizi kwenye nchi majirani: UNHCR

Zaidi ya wasyria nusu milioni sasa ni wakimbizi kwenye nchi majirani: UNHCR

Idadi ya raia wa Syria waliokimbia na kuingia nchi majirani kwa sasa imepita watu nusu milioni kwa mujibu wa Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR. UNHCR inasema kuwa karibu wasyria 510,000 wamesajiliwa au wanaendelea kusajiliwa nchini Lebanon, Iraq, Uturuki na Kaskazini mwa Afrika.

UNHCR inasema kuwa chini ya nusu ya wakimbizi waliosajiliwa wanaishi kwenye makambi huku idadi kubwa wakiishi nje ya makambi kwenye nyumba za kukodisha au kwa watu wengine. Wakimbizi wa Syria kwa sasa wamechukua hifadhi kwenye kambi 14 nchini Uturuki, kambi mbili nchini Iraq na tatu nchini Jordan. Melissa Fleming ambaye ni msemaji wa UNHCR anasema kuwa takriban wakimbizi 3000 kutoka Syria wanasajiliwa kila siku mipakani.

Jordan inakadiria kuwa ina watu 100,000 nchini mwake ambao hawajasajiliwa. Uturuki inakadiria kuwa kuna zaidi ya wakimbizi 70,000 walio nje ya makambi na Misri inakadiria idadi kama hiyo ikisema kuna wasyria 70,000 nchini mwake ambao hawajasajiliwa. Lebanon maelfu bado hawajasajiliwa. Tunashuhudia watu zaidi wanaowasili, wazee, watoto walio chini ya maiaka 18 wakiwemo watoto wachanga waliozaliwa usiku wa tarehe 9 mwezi huu. Pia tunagundua kuna watoto wasoi na wazazi wanaovuka mpaka. Hawa ndio watoto wanaohitaji msaada zaidi.