Misaada zaidi yahitajika Syria wakati wa baridi kali; hospitali zaharibiwa: Mashirika ya UM

23 Novemba 2012

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema hivi sasa linakusanya zaidi ya vifurushi Laki moja vya nguo za watoto wa wakimbizi huko Syria wakati huu ambapo msimu wa baridi kali unawadia.

Msemaji wa UNICEF Marixie Mercado amesema wanakusanya pia  mablanketi Laki Moja na Sitini ikiwemo ya watoto hao wa wakimbizi pamoja na wengine waliopote makazi yao nchini Syria.

Katika hatua nyingine shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema hadi sasa limeshasambaza vifurushi vya misaada kwa familia 60,300 nchini Syria ambavyo vimenufaisah zaidi ya watu Laki Tatu.

Msemaji wa NHCR Adrian Edwards amesema msaada huo umetolewa wakati huu ambapo idadi ya wakimbizi wa Syria waliotafuta hifadhi katika maeneo mbali mbali kwenye eneo hilo wakifikia zaidi  ya Laki Nne na Elfu Arobaini na Mbili.

Wakati huo huo shirika la Afya duniani, WHO limesema idadi kubwa ya hospitali na vituo vya afya kwenye mji mkuu wa Syria, Damascus vimeharibiwa huku kukiwepo na wajawazito wengi wanaohitaji upasuaji wa kujifungua na wana hofu ya kuchelewa kufika hospitali mapema kwa ajili ya kujifungua.

Tarik Jasarevic ni Msemaji wa WHO;

(SAUTI YA JASAREVIC)