Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wanaathiriwa na machafuko yalooenea DRC: UM

Watoto wanaathiriwa na machafuko yalooenea DRC: UM

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto na maeneo ya vita vya silaha, Leila Zerrougui, ameelezea kusikitishwa kwake kuhusu hali ya watoto katika mzozo unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, DRC.

Kuingia kwa waasi wa M23 katika miji ya Goma na Sake, kumeambatana na ukiukaji mkubwa unaotekelezwa dhidi ya watoto. Bi Zerrougui amesema watoto wameuawa na kujeruhiwa katika mapigano, wakilengwa makusudi na pia yadaiwa wanatumiwa kama wanajeshi.

Katika kipindi cha siku nne zilizopita, watoto kumi na sita, wakiwemo mtoto mwenye miaka miwili, wamejeruhiwa kwa risasi na vilipuzi wakati wa mapigano kati ya M23 na vikosi vya usalama.

Bi Zerrougui ametoa wito kwa pande zote zinazozozana kusitisha mapigano mara moja na kuaepusha watoto na athari za vita hivyo, akisema kuwa jamii ya kimataifa haiwezi kuvumilia kuona wimbi jingine la dhuluma dhidi ya watoto bila watu kuwajibika.