Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalam wa UM ahofia vitisho dhidi ya majaji Sri Lanka

Mtaalam wa UM ahofia vitisho dhidi ya majaji Sri Lanka

Mtaalam wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa majaji na wanasheria, Gabriela Knaul, leo ameelezea wasiwasi wake kuhusu ripoti za vitisho dhidi ya majaji na maafisa wa sheria nchini Sri Lanka, na kuonya kuwa huenda vitisho hivyo vikawa miongoni mwa mashambulizi na ulipizaji kisasi wanaokumbana nayo wanasheria.

Bi Knaul amesema vitisho hivyo ni sehemu ya kuingilia uhuru wa mfumo wa haki nchini humo, na hivyo kuitaka serikali ya Sri Lanka kuchukua hatua kuhakikisha kuwa hadhi ya vyombo vya sheria inalindwa, na kuwaruhusu wanasheria kutekeleza majukumu yao ya kitaaluma bila vizuizi, mashinikizo, na vitisho, chini ya wajibu wa taifa hilo katika sheria za kimataifa za haki za binadamu.

Kwa mujibu wa ripoti zilizopokelewa na mtaalam huyo wa haki za binadamu, mashambulizi mengi na uingiliaji wa kazi ya vyombo vya sheria nchini Sri Lanka havifanyiwi uchunguzi mzuri, na wanaovitekeleza hawawajibiki.