Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wakumbuka wafanyakazi wake waliokufa kazini:Ban

UM wakumbuka wafanyakazi wake waliokufa kazini:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amewaandikia wafanyakazi wote wa Umoja wa Mataifa akielezea huzuni yake kufuatia vifo ya wafanyakazi wa Umoja huo hivi karibuni.

Vifo hivyo ni pamoja na vya wafanyakazi 7 waliokufa kwenye shambulio kwenye ofisi za Umoja wa mataifa mjini Mazar-i-Sharif nchini Afghanistan, 32 kwenye ajali ya ndege mjini Kinshasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hapo jana pamoja na katika matukio mengine nchini Ivory Coast na Haiti. Jumla ya wafanyakazi 41 wa Umoja wa Mataifa wamekufa katika matukio hayo tofauti.

Ban amesema fikra na sala za Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wote ziko pamoja na familia za waliofariki dunia wakitekeleza majukumu yao, waliopoteza marafiki na pia wafanyakazi wenzetu. Ameongeza kuwa ana uhakika wafanyakazi waliopoteza maisha yao wangependa Umoja wa Mataifa kuendelea na kazi walioifanya kwa moyo wote walipokuwa hai.

Kwa kutambua mchango wao Ban ameziomba ofisi zote za Umoja wa Mataifa duniani kupeperusha bendera nusu mlingoti Jumatano April 6, siku ambayo pia kwa kushirikiana na wafanyakazi wa makao makuu New York watafanya hafla ya kuweka mashada ya maua mahsusi kwa ajili ya kuwakumbuka wafanyakazi hao , saa tatu asubuhi saa za New york.