Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laelezea kujitolea kwake kuisaidia Somalia

Baraza la Usalama laelezea kujitolea kwake kuisaidia Somalia

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limeazimia kwa kauli moja kukaribisha kuhitimishwa kipindi cha mpito nchini Somalia. Baraza hilo la Usalama pia limeelezea kujitolea kwake kufanya kazi kwa karibu na taasisi za taifa hilo, na kutoa wito kwa rais mpya wa Somalia kuunda serikali inayowahusisha wote.

Baraza la Usalama limekaribisha kuundwa kwa taasisi mpya, ikiwemo bunge, na limetoa wito kwa serikali iwajibike zaidi katika masuala ya haki za binadamu, uongozi wa kisheria na kukabiliana na ufisadi. Hata hivyo, mwisho wa kipindi cha mpito nchini Somalia ndio mwanzo tu, amesema Balozi wa Uingereza kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Mark Lyall Grant, katika mkutano na waandishi wa habari.

Balozi Grant amesema azimio lililopitishwa na Baraza la Usalama linatoa wito kwa jamii ya kimataifa kuwa na mwelekeo mwema zaidi katika kuisadia Somalia.

"Kwa kukamilisha kipindi cha mpito, Somalia sasa ina fursa ya kuelekea kwenye siku za usoni zenye amani. Lakini mwisho wa kipindi cha mpito ni mwanzo tu. Somalia bado inakabiliwa na tishio kubwa kutoka kwa wanamgambo wa al-shabaab. Azimio hili linaonyesha shukran za Baraza la Usalama kwa mchango wa AMISOM katika kuimarisha hali ya usalama , lakini tusije tukalegea”